Rais wa Sudan: Matakwa ya wananchi wanaoandamana ni halali
Rais Omar al Bashir wa Sudan amekiri kuwa matakwa yanayoshinikizwa na wananchi wa nchi hiyo ambao wamekuwa wakishiriki maandamano dhidi ya serikali kwa miezi kadhaa sasa ni halali.
Bashir aliyasema hayo jana katika hotuba yake ya kwanza Bungeni tangu atangaze hali ya hatari mnamo Februari 22 ambapo amebainisha kuwa, "Mgogoro wa kiuchumi umeathiri idadi kubwa ya wananchi."
Hata hivyo Rais wa Sudan amevilaumu vyama vya upinzani kwa kuchochea kile alichokitaja kama ghasia ambazo zimesababisha makumi ya watu kuuawa.
Bashir amefafanua kuwa, "Baadhi ya makundi ya kisiasa yanatumia haya (maandamano) kuchochea chuki katika jamii, jambo ambalo limefanya tupoteza idadi kubwa ya watu."
Maandamano ya kupinga serikali ya Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan yameendelea kushuhudiwa katikaka miji mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Khartoum, tokea katikati ya mwezi Desemba mwaka jana hadi sasa.
Makumi ya waandamanaji ambao wanataka Rais Omar al-Bashir ang'atuke madarakani wametiwa mbaroni, huku ripoti za asasi za kiraia zikieleza kuwa watu zaidi ya watu 50 wameuawa hadi sasa katika ghasia na machafuko huko Sudan.
Maandamano hayo yaliyoanza kwa kulalamikia ughali wa maisha yalibadilika na kuwa wimbi la kumtaka Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani, lakini bado anashikilia msimamo wake wa kubakia uongozini.