Watu 20 wauawa na 'watu wenye sare za kijeshi' Nigeria
Kwa akali watu 20 wameuawa baada ya watu waliokuwa wamevalia magwanda ya kijeshi kushambulia kijijini kimoja katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria.
Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, wavamizi hao waliokuwa wamebeba mapanga na bunduki aina ya AK-47 walishambulia kijiji cha Ungwan Aku katika jimbo la Kaduna, kilichoko katikati ya Nigeria jioni ya jana Jumatatu, ambapo watu wengine wengi wameripotiwa kujeruhiwa.
Wakazi wa kijiji hicho wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na hofu ya kushambuliwa tena, baadhi yao wakikimbilia kwenye msitu wa karibu. Watu wasiopungua 95 waliuawa katika mashambulizi mengine ya silaha katika jimbo hilo la Kaduna mwezi Februari mwaka huu.
Mauaji haya ya Kaduna yanajiri wiki moja baada ya watu 50 kuuawa katika shambulio jingine la wavamizi waliobeba silaha kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Kwa mujibu Spika wa Bunge la Jimbo la Zamfara, Sunusi Rikiji, mauaji hayo yalifanyika Jumanne iliyopita katika kijiji cha Sakajiki, eneo la Kauran Namoda jimboni Zamfara.
Mwezi uliopita, wavamizi waliokuwa juu ya pikipiki waliwaua kwa kuwapiga risasi watu 32 katika kijiji cha Kware, wilayani Shinkafi katika jimbo hilo hilo la Zamfara.