Magaidi wa Daesh watumia mapigano mapya Libya kuendeleza ukatili
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52743-magaidi_wa_daesh_watumia_mapigano_mapya_libya_kuendeleza_ukatili
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limetumia ombwe lililosababishwa na mapigano kati ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa na vile vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar nchini Libya, kuanzisha wimbi jipya la mauaji nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 10, 2019 02:26 UTC
  • Magaidi wa Daesh watumia mapigano mapya Libya kuendeleza ukatili

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limetumia ombwe lililosababishwa na mapigano kati ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa na vile vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar nchini Libya, kuanzisha wimbi jipya la mauaji nchini humo.

Kundi hilo limetangaza kuhusika na mauaji ya watu watatu katika shambulio la jana Jumanne katika mji wa Fuqaha ulioko kusini mwa Tripoli.

Kadhalika mtu mmoja ameripotiwa kutekwa nyara na magaidi hao katika mji huo wa jangwani, unaodhibitiwa na vikosi vitiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar.

Huku hayo yakijiri, idadi ya watu waliouawa katika mapigano kati ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa na vile vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar nchini Libya imeongezeka na kufikia watu 47.

Msafara wa magari ya kijeshi ya askari wa Jenerali Haftar ukilekea Tripoli

Hayo yalisemwa jana Jumanne na Tarik Jasarevic, msemaji wa Shirika la Afya Duniani WHO mjini Geneva, ambapo aliongeza kuwa watu wengine 180 wamejeruhiwa katika makabiliano hayo ya 'kugombania mji mkuu Tripoli'.

Mapigano hayo  ambayo yamezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia wa Tripoli yamehatarisha juhudi za kieneo na kimataifa za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya kupitia njia ya mazungumzo na utatuzi wa kisiasa.