Apr 10, 2019 07:46 UTC
  • Kongamano la 'amani na uchaguzi' Libya laakhirishwa kutokana na mapigano

Mkutano wa kujadili mgogoro wa Libya na maandalizi ya uchaguzi ujao nchini humo uliotazamiwa kufanyika kati ya Aprili 14 na 16 magharibi mwa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta umeakhirishwa kutokana na kushadidi mapigano kati ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa na vile vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar.

Hayo yalitangazwa jana Jumanne na Ghassan Salame, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya na kuongeza kuwa, "Mkutano huo umeakhirishwa kutokana na mapigano. Hatuwezi kuwaambia watu washiriki mkutano huo huku milio ya risasi na hujuma za anga zikiendelea kurindima."

Bila kuanisha tarehe au siku, mwanadiplomasia huyo wa UN katika masuala ya Libya amesema mkutano huo uliokuwa umepangwa kufanyika katika mji wa Ghadames, kusini magharibi mwa nchi utafanyika hivi karibuni. 

Huku hayo yakijiri, idadi ya watu waliouawa katika mapigano kati ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa na vile vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar nchini Libya imeongezeka na kufikia watu 47, huku wengine 180 wakijeruhiwa katika makabiliano hayo ya 'kugombania mji mkuu Tripoli'.

Wakuu wa Libya waliposhiriki mkutano wa amani Italia miezi michache iliyopita

Mapigano hayo  ambayo yamezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia wa Tripoli yamehatarisha juhudi za kieneo na kimataifa za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya kupitia njia ya mazungumzo na utatuzi wa kisiasa.

Awali uchaguzi mkuu nchini humo ulikuwa umepangwa kufanyika Disemba 10 mwaka jana 2018 lakini zoezi hilo liliahirishwa kutokana mpasuko uliojitokeza baina ya viongozi wa mirengo hasimu ya kisiasa na wimbi la mapigano na machafuko yaliyozuka katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Tags