Machar asema ni muhali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52815-machar_asema_ni_muhali_kuunda_serikali_ya_umoja_wa_kitaifa_sudan_kusini
Kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini, Riek Machar amesema ni vigumu kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kufikia Mei 12 kama ilivyopangwa chini ya makubaliano ya amani ya Addis Ababa kati yake na Rais Salva Kiir.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 13, 2019 03:04 UTC
  • Machar asema ni muhali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Sudan Kusini

Kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini, Riek Machar amesema ni vigumu kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kufikia Mei 12 kama ilivyopangwa chini ya makubaliano ya amani ya Addis Ababa kati yake na Rais Salva Kiir.

Machar aliyasema hayo jana Ijumaa katika mahojiano na shirika la habari la Reuters na kuongeza kuwa, anatumai Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan litaendelea kuidhaminia usalama Sudan Kusini.

Juzi Alkhamisi mahasimu hao wawili wa kisiasa wa Sudan Kusini walikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu mwezi Septemba mwaka jana, katika mkutano wa Vatican, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki mjini Rome, Italia.

Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani ambaye alikuwa mwenyeji wa viongozi hao amemuomba Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir pamoja na hasimu wake Riek Machar kuendeleza mazungumzo ya amani licha ya ugumu wake.

Viongozi wa Sudan Kusini walipokutana na Papa

Hii ni katika hali ambayo, Machar anatazamiwa kurejea nchini Sudan Kusini mwezi ujao, chini ya makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwezi Septemba mwaka jana huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, nakuchukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Nchi ya Sudan Kusini iliyojitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani, Disemba mwaka 2013 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni wamelazimika kuwa wakimbizi.