Sudan Kusini inataka uanachama wa WTO kustawisha uchumi wake
Serikali ya Sudan Kusini imetangaza azma yake ya kujiunga na Shirika la Biashara Duniani ,WTO, ili kuimarisha uchumi wake baada ya kumalizika vita vya muda mrefu nchini humo.
Naibu waziri wa biashara na mambo ya Afrika Mashariki Bw. Mou Mou Athian amesema, baada ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC mwaka 2016, Sudan Kusini imekuwa ikitafuta uanachama katika Shirika la Biashara Duniani WTO, hatua ambayo itafungua mlango wa nchi hiyo kupata mitaji na soko kwa bidhaa za kienyeji.
Amebaini kuwa kushiriki Sudan Kusini kwenye biashara ya kikanda na kimataifa kutachangia utulivu wa kijamii na kiuchumi, ambao utaboresha usalama wa nchi hiyo baada ya mgogoro uliodumu kwa miaka mitano.
Athian amesema Sudan Kusini inahitaji kuwa wazi na kuunganishwa na sehemu nyingine za dunia kama sharti la kuchochea na kudumisha ukuaji wa uchumi unaohitajika katika kukuza utulivu wa kijamii na kiuchumi.
Nchi ya Sudan Kusini iliyojitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani, Disemba mwaka 2013 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni kulazimika kuwa wakimbizi. Mapatano ya amani baina ya mahasimu nchini humo yamefikiwa hivi karibuni lakini bado yanalegalega