Misri yatangaza tarehe ya kura ya maoni ya kurefusha uongozi wa Sisi
Tume ya Uchaguzi ya Misri imetangaza tarehe ya kura ya maoni yenye azma ya kuondoa kikomo cha muhula wa rais, hatua ambayo huenda ikamruhusu Rais Abdulfattah al-Sisi wa nchi hiyo kugombea zaidi ya mihula miwili inayoruhusiwa na katiba.
Tume hiyo ilitoa tangazo hilo hapo jana Jumatano na kubainisha kuwa, zoezi hilo la kura ya maoni litafanyika kati ya Aprili 20 na 22.
Tangazo hilo limetolewa siku moja tu baada ya Bunge la Misri kupasisha muswada unaoruhusu kukifanyia marekebisho kipengee cha 140 cha katiba, ambacho kinasema rais anapaswa kugombea mihula miwili pekee ya miaka minne minne.
Iwapo wananchi wa Misri watayaunga mkono marekebisho hayo ya katiba kwa wingi wa kura katika kura hiyo ya maoni, huenda Sisi akabakia madarakani hadi mwaka 2030.
Muungano wa upinzani nchini Misri hata hivyo umekosoa vikali mpango huo wa kuondoa kikomo cha muhula wa rais, ukisisitiza kuwa marekebisho hayo ya katiba yatavunja misingi ya uhuru, dekomkrasia na uwepo wa utawala wa kiraia.
Muungano huo umesema iwapo marekebisho hayo ya katiba yatapasishwa na kutekelezwa, itakuwa ndio kwanza milango ya udikteta na ubabe imefunguliwa.
Hii ni katika hali ambayo, serikali ya al-Sisi imekuwa ikikosolewa kwa kuwakandamiza wapinzani na hasa viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin sambamba na kuviwekea mbinyo vyombo vya habari, tangu kiongozi huyo ashike hatamu za uongozi kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013.