Wanamgambo kadhaa wa Rwanda wakamatwa nchini Burundi
Serikali ya Burundi imetangaza habari ya kuwatia mbaroni wanamgambo saba wa Rwanda na kisha kuwakabidhi kwa serikali ya Kigali.
Duru za habari zimearifu kuwa, serikali ya Burundi iliwakamata wapiganaji hao wa Rwanda mpakani mwa nchi mbili hizo, na kuwakabidhi kwa mamlaka husika nchini Rwanda.
Inaarifiwa kuwa, jumuiya za kieneo kwa ushirikiano na jeshi la polisi la Burundi zimewakabidhi waasi hao kwa mamlaka husika nchini Rwanda baada ya kukamatwa na jeshi la Burundi mpakani mwa nchi mbili hizo.
Haya yanajiri katika hali ambayo, serikali ya Rwanda hapo jana ilitangaza kuwa imemkamata mkuu wa kundi la waasi la NFL, Callixte Nsabimana ambaye pia anajulikana kama Sankara.
Burundi na Rwanda zimekuwa katika mzozo tangu kulipojiri jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza hapo tarehe 13 Mei 2015.
Serikali ya Nkurunziza imekuwa ikiituhumu Rwanda kuwa inaunga mkono magenge hayo ya waasi yanayovuruga usalama wa nchi hiyo.