Walibya waandamana mjini Tripoli kuulaani utawala wa Saudi Arabia
Raia wa Libya wamefanya maandamano mbele ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tripoli, wakilaani uingiliaji haribifu wa Riyadh katika masuala ya ndani ya nchi yao.
Waandamanaji hao waliopiga kambi mbele ya ubalozi wa Saudia mjini Tripoli wamekosoa vikali kitendo cha Riyadh kuwaunga mkono wanamgambo wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya wanaoungwa mkono na Khalifa Haftar. Hii ni katika hali ambayo mji wa Misrata pia ulishuhudia maandamano ya kulaani hujuma za wapiganaji wa Haftar na waungaji mkono wake dhidi ya mji wa Tripoli. Baadhi ya washiriki wa maandamano hayo waliovalia vizibao vya rangi ya njano pia wamelaani uungaji mkono wa serikali ya Ufaransa kwa wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar.
Wakati huo huo habari zinaelezea kujiri mapigano makali katika mji wa Sabhā, kusini magharibi mwa Libya. Operesheni za kijeshi za wapiganaji wa Haftar mjini Tripoli ambazo zilianza yapata mwezi mmoja uliopita, zimepelekea hadi sasa watu elfu 55 kuwa wakimbizi. Kwa miaka kadhaa sasa wapiganaji wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya chini ya jenerali huyo wamekuwa wakiungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi zikiwemo Marekani na Ufaransa. Wapiganaji hao wamekuwa wakisonga mbele katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Hivi karibuni gazeti la Kimarekani la The Wall Street Journal liliandika kuwa ni baada ya Khalifa Haftar kufanya safari mjini Riyadh, Saudia ndipo akaanzisha mashambulizi makali dhidi ya mji wa Tripoli akitaka kuudhibiti mji huo.