May 08, 2019 13:45 UTC
  • Mapigano katika mji ulioathiriwa na Ebola DRC yaua watu 9

Kwa akali watu tisa wameripotiwa kupoteza maisha katika mapigano baina ya askari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wanamgambo waliobeba silaha katika mji wa Butembo ulioathiriwa na ugonjwa hatari wa Ebola.

Meya wa mji huo, Sylvain Kanyamanda Mbusa amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, wanamgambo wanane na askari polisi mmoja wameuawa katika mapigano hayo ya leo Jumatano, katika mji huo ulioko mashariki mwa nchi.

Amesema maafisa usalama wamefanikiwa kuzima jaribio la wanamgambo hao kuuvamia mji huo, na kwamba kadhaa miongoni mwao wametiwa mbaroni.

Juhudi za kupambana na ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeendelea kukabiliwa na vizingiti kutokana na makundi hayo ya wanamgambo kushambulia vituo vya afya vinavyotoa matibabu kwa wagonjwa wa maradhi hayo.

Madaktari wakiwatibu waathiriwa wa Ebola mashariki mwa DRC

Mwezi uliopita, madaktari wa Kongo DR walitishia kuitisha mgomo iwapo maafisa usalama hawatawadhaminia usalama madaktari wanaotoa matibabu kwa waathiriwa wa Ebola mashariki mwa nchi. Hii ni baada ya daktari wa Shirika la Afya Duniani WHO raia wa Cameroon aliyekuwa akitibu wagonjwa wa Ebola kuuawa katika uvamizi wa wanamgambo hao katika mji huo wa Butembo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, watu zaidi ya 1000 wameaga dunia kutokana na maradhi ya Ebola nchini humo tangu ugonjwa huo hatari uibuke upya Agosti mwaka jana.

Tags