UN yatahadahrisha kuwa magaidi wa Al Shabab wamebadilisha mbinu
(last modified Sun, 19 May 2019 07:56:38 GMT )
May 19, 2019 07:56 UTC
  • UN yatahadahrisha kuwa magaidi wa Al Shabab wamebadilisha mbinu

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa magaidi wa kundi la Al Shabab sasa wamebadilisha mbinu zao ili kuwawezesha kutekeleza mashambulizi mengi na hatari zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa, hivi sasa magaidi wakufurishaji wa Al Shabab hawategemei mabomu ya kawaida ya kijeshi ambayo wanalazimika kuyanunua katiko soko la kimataifa bali wamepata uwezo wa kujiundia mabomu. Kutokana na uwezo huo, magaidi wa Al Shabab sasa wanatazamiwa kutekeleza mashambulizi mengi na yenye kusababisha vifo.

Taarifa hiyo imebaini kuwa, katika mwaka huu wa 2019, magaidi wa Al Shabab wametekeleza mashambulizi kadhaa nchini Somalia licha ya oparesheni za Jeshi la Somalia na washirika wake wa kimataifa za kujaribu kuangamiza kundi hilo la kigaidi.

Wataalamu wa mabomu wanasema kuna uhusiano baina ya uwezo wa al Shabab wa kujiundia mabomu na ongezeko la mashambulizi makubwa katika mji mkuu Mogadishu.

Magaidi wa Al Shabab

Ripoti hiyo imechapishwa baada ya wataalamu kuchunguza mashambulizi 20 yaliyotekelezwa na magaidi wakufurishaji wa Al Shabab tokea Julai 2018.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi karibuni imshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wakufurishaji wa Al Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wanaokadiriwa kuwa 21,000 wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa Al Shabab. Wanajeshi wa Amisom walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone.

 

Tags