Kamanda mwingine mwandamizi wa al-Shabaab ajisilimisha kwa serikali Somalia
Katika kile kinachoonekana ni kuendelea kuparaganyika kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab, kamanda mwingine mwandamizi wa kundi hilo la ukufurishaji la Somalia amejisalimisha kwa serikali.
Hayo yamesemwa na Mohammad Hassan, kamanda mkuu wa Kikosi cha 43 cha jeshi la Jubaland na kuongeza kuwa, gaidi huyo kwa jina Sidow Abdi Gedi alijisalimisha jana Jumapili kwa vyombo vya usalama katika mji bandari wa Kismayo, katika eneo la Lower Juba.
Afisa huyo wa jeshi la Jubaland amesema wako tayari kuwapokea wanamgambo wote wanaojisalimisha, huku akionya kuwa operesheni zao zitafuta kikamilifu magaidi hao katika eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kujisalimisha, kamanda huyo wa ngazi za juu wa al-Shabaab amesema, "Nimeamua kuachana na kundi hili baada ya kujiunga nalo miaka saba iliyopita, kwa kuwa nataka kupata utulivu wa nafsi na kuishi kwa amani na wanajamii wengine."
Mapema mwezi huu, makamanda wengine wa al-Shabaab waliliasi kundi hilo la ukufurishaji na kujisalimisha kwa vyombo vya dola katika eneo la Gedo.
Mwaka 2017, Mukhtar Robow, aliyekuwa msemaji wa al-Shabaab na ambaye pia alikuwa miongoni mwa viongozi wenye vyeo vya juu kwenye kundi hilo alijisalimisha kwenye mikono ya serikali, pamoja na wapiganaji wake kadhaa katika mji uliopo kusini magharibi mwa Hudur.