Indhari ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali inavyozidi kuwa mbaya nchini Libya
Kuendelea vita nchini Libya kumezidisha machafuko na mgogoro katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kiasi kwamba Ghassan Salamé, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kabisa kwamba, hatoi tahadhari kuhusu kutokea vita vya ndani na vya umwagaji damu tu, bali anatoa onyo la kusambaratika vipande vipande Libya.
Mwakilishi huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ameongeza kuwa, vita vya ndani nchini humo vinaweza kupelekea Libya igawike vipande vipande na kuwa vijinchi vidogo vidogo hasimu.
Moto wa mgogoro wa Libya ulirindima zaidi kuanzia tarehe 4 Aprili mwaka huu wa 2019 baada ya Jenerali Khalifa Haftar kutoa amri ya kushambuliwa mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli na kuvuruga juhudi zote za upatanishi wa mgogoro wa Libya. Jenerali Haftar alianzisha vita hivyo kwa baraka na uungaji mkono kamili wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baada ya kuzungumza na simu na rais wa Marekani, Donald Trump kwa tamaa kwamba angeliweza kuuteka haraka sana mji wa Tripoli. Hata hivyo jenerali huyo hakutarajia kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa ingeliweza kusimama kidete kukabiliana naye kiasi kwamba muqawama wa wanajeshi wa serikali hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa umefuta ndoto za Jenerali Khalifa Haftar za kuuteka haraka mji wa Tripoli. Sasa hivi miezi karibu miwili inapita na bado vita vinaendelea.
Ghassan Salamé amesema kuwa, anatumai baadhi ya pande zinazodhani kuwa njia ya kijeshi ndiyo itakayotatua mgogoro wa Libya, zitaachana na fikra zao hizo potofu.
Wimbi jipya la vita huko Libya limezusha maafa ya kibinaadamu katika maeneo mengi ya Libya na hivi sasa nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika imezama kwenye migogoro mingi. Kuzuka tena magaidi wa Daesh (ISIS) na kupata nguvu katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa Libya ni miongoni mwa hatari kubwa za kiusalama zilizosababishwa na wimbi hilo jipya la mapigano. Hii ni kwa sababu, wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar wamelazimika kuondoka maeneo ya kusini mwa nchi hiyo ili kwenda kutia nguvu mashambulizi ya Tripoli. Kuondoka kwao huko kusini mwa Libya kumetoa mwanya kwa makundi ya kigaidi kama Daesh na al Qaida kupata nguvu na kujitokeza tena katika maeneo hayo kiasi kwamba sasa bendera za Daesh zinaonekana kupepea katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa Libya. Shambulizi la magaidi wa ISIS katika kisima cha mafuta cha Zueitina huko Zellah ni hatari nyingine iliyosababishwa na uamuzi wa Jenerali Khalifa Haftar wa kuushambulia mji mkuu wa Libya, Tripoli. Mji wa Zella uko umbali wa kilomita 650 kusini mashariki mwa Tripoli na una visima vitano vikubwa vya mafuta. Hadi hivi sasa magaidi wa Daesh wameshafanya mashambulizi kadhaa ya kujaribu kudhibiti visima vya mafuta vya eneo hilo.
Mustafa San'uLlah, mkuu wa Shirika la Taifa la Mafuta la Libya amesema kuwa, kama hali nchini humo itaendelea vivi hivi, basi Libya itapoteza asilimia 95 ya uzalishaji wake wa mafuta.
Kuongezeka uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya Libya ikiwa ni pamoja na madola hayo kuzisheheneza kwa silaha pande hazimu, ni jambo jingine baya lililosababishwa na uamuzi wa Jenerali Khalifa Haftar wa kuanzisha vita dhidi ya Tripoli. Baadhi ya madola ajinabi hasa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na Ufaransa si tu zimetangaza waziwazi uungaji mkono wao kwa Jenerali Khalifa Haftar, bali pia yamemsheheneza silaha chungu nzima na zana nyingine za kijeshi jenerali huyo muasi.
António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea kusikitishwa sana na operesheni za kijeshi zinazoendelea hivi sasa huko Libya na kuyataka madola ya kigeni yaheshimu marufuku ya silaha iliyowekewa nchi hiyo.
Kiujumla ni kwamba hali ya nchini Libya hivi sasa ni mbaya. Magenge ya kigaidi yanazidi kupata nguvu na vita vimeenea katika ufukwe wote wa Bahari ya Mediterranean na kuhatarisha usalama wa hata nchi zinazopakana na Libya. Baya zaidi ni hatari ya kugawika vipande vipande nchi hiyo na kupotea kabisa utambulisho wake wa nchi moja. Maafisa wengi wa kimataifa na wataalamu wa masuala ya Libya wanatahadharisha kuhusu hatari ya kuendelea vita nchini humo na kuyataka madola ajinabi yaache kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ili iwezekane kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo.