Ripoti: Watu milioni 10 Afrika Mashariki wanavuta bangi, Tanzania yaongoza
(last modified Sat, 25 May 2019 10:24:25 GMT )
May 25, 2019 10:24 UTC
  • Ripoti: Watu milioni 10 Afrika Mashariki wanavuta bangi, Tanzania yaongoza

Utafiti mpya umefichua kuwa, takriban watu milioni 10 katika kanda ya Afrika Mashariki wanavuta bangi kinyume cha sheria, huku Tanzania ikishika nafasi ya kwanza katika orodha hiyo.

Ripoti mpya ya shirika la Africa Regional Hemp & Cannabis ya mwaka huu 2019 imebainisha kuwa, watu milioni 3.6 nchini Tanzania wanatumia bangi kinyume cha sheria za nchi, kutokana na sababu mbalimbali. Tanzania inashika nafasi ya tano barani Afrika katika ripoti hiyo.

Kenya imeorodheshwa katika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wavuta bangi katika eneo la Afrika Mashariki, ambapo watu milioni 3.3 wanatumia mmea huo wa kulevya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Uganda ina watu milioni 2.6 wanaotumia mmea huo kutokana na sababu mbalimbali. Burundi na Sudan Kusini hazijatajwa kwenye ripoti hiyo.

Askari wakifyeka mashamba ya bangi Tanzania

Ripoti hiyo mpya ya shirika la Africa Regional Hemp & Cannabis ya mwaka huu 2019 imesema kuna watumiaji bangi wapatao milioni 83 barani Afrika, huku Nigeria ikiongoza kwa milioni 20.8, Ethiopia milioni 7.1, Misri milioni 5.9  huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikifuata kwa kuwa na wavuta bangi milioni 5. 

Nchi ambazo hazina wavutaji bangi wengi barani Afrika kwa mujibu wa ripoti hiyo ni Zimbabwe milioni 1.1, Malawi milioni 1.2, Niger milioni 1.2 na Zambia milioni 1.4.

 

Tags