Wanajeshi 25 wa Nigeria wauawa katika hujuma ya magaidi wa Boko Haram
Wanajeshi 25 wa Nigeria wameuawa katika hujuma ya kuvizia ambayo imetekelezwa na magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram.
Duru zinaarifu kuwa wanajeshi 25 wameuawa pamoja na raia kadhaa katika hujuma ya kuvizia iliyotekelezwa na magaidi wa Boko Haram Jumamosi asubuhi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa zinasema magaidi waliwafyatulia risasi askari waliokuwa wakiwasindikiza raia waliookolewa kutoka kijiji kimoja katika jimbo la Borno ambalo ni ngome ya magaidi hao wa Boko Haram.
Uasi na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram yalianza mwaka 2009 katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria na kisha baadaye kupanua wigo wa mashambulio yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon.

Hadi sasa mashambulio hayo yameshasababisha zaidi ya watu elfu ishirini na tano kuuawa na wengine karibu milioni tatu kubaki bila makazi na hivyo kulazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amekuwa akiahidi kila mara kuchukua hatua kali za kupambana na kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haram, lakini hadi sasa ameshindwa kutimiza ahadi yake hiyo, na hivyo kukabiliwa na ukosoaji ndani na nje ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.