Mapigano yaibuka upya jimboni Yei nchini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53784-mapigano_yaibuka_upya_jimboni_yei_nchini_sudan_kusini
Mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa kundi la waasi la National Salvation Front (NAS) linaloongozwa na Jenerali Thomas Cirillo yameibuka upya katika mkoa wa Yei nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 29, 2019 03:36 UTC
  • Mapigano yaibuka upya jimboni Yei nchini Sudan Kusini

Mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa kundi la waasi la National Salvation Front (NAS) linaloongozwa na Jenerali Thomas Cirillo yameibuka upya katika mkoa wa Yei nchini Sudan Kusini.

Msemaji wa kundi hilo, Suba Samuel amesema vikosi vya serikali ndivyo vilivyozusha mapigano hayo katika maeneo ya Lanyia na Wonduruba. Amesema mapigano hayo yalianza Jumapili iliyopita ya Mei 26. 

Hakuna taarifa iliyotolewa na serikali ya Juba kufikia sasa kuhusu mapigano hayo, wala idadi ya wahanga wa makabiliano hayo kati ya vikosi vya serikali na waasi.

Mapema mwezi huu, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini aliwataka viongozi wote wa upinzani kuchukua hatua za kivitendo katika kutekeleza makubaliano ya amani, ili kurejesha matumaini na matarajio ya wananchi.

 

Mji wa Yei nchini Sudan

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.