Upinzani Malawi kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani
Kinara wa chama kikuu cha upinzani cha Malawi Congress (MCP) amesema atawasilisha faili mahakamani kupinga 'wizi wa kura' katika uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo hivi karibuni.
Lazarus Chakwera aliyasema hayo jana Ijumaa na kufafanua kuwa, "Ninapinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyochakachuliwa ya Tume ya Uchaguzi na nitawasilisha kesi ya kupinga wizi huo wa kura katika Mahakama Kuu."
Ameeleza bayana kuwa, "Kile tulichoshuhudia mbele ya macho yetu sio uchaguzi, bali ni wizi wa mchana wa kura na jinai dhidi ya taifa letu na demokrasia yetu."
Kwa mujibu wa matokeo ya Tume ya Uchaguzi yalitolewa Jumatatu iliyopita, Peter Mutharika aliibuka mshindi na kuhifadhi kiti chake cha urais, huku akimshinda Chakwera kwa kura 159,000 pekee.

Mutharika aliapishwa siku moja baada ya kutolewa matokeo hayo yaliyokuwa yamecheleweshwa na Tume ya Uchaguzi ya nchii hiyo, lakini alitawazwa rasmi kuliongoza taifa hilo kwa muhula mwingine jana Ijumaa katika Uwanja wa Kitaifa wa Kamuzu katika eneo la Blantyre.
Kabla ya hapo, Mahakama Kuu ilitoa agizo la kusitishwa utangazaji wa matokeo ya kura ya rais na kutoa maelekezo ya kuhesabiwa upya kwa kura za theluthi ya maeneo yaliyoshiriki uchaguzi, kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na chama cha MCP.
Wananchi wa Malawi Jumanne ya Mei 22 walijitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu huo ambapo Rais Peter Mutharika alikabiliwa na ushindani mkali.