Rwanda yaitaka Burundi iwashughulike wahalifu 6,000 wa mauaji ya kimbari
Mwendesha mashtaka mkuu wa Rwanda Jean Mutangana ametoa wito kwa nchi jirani ya Burundi kushughulikia watu ambao amedai walihusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda dhidi ya Watutsi.
Akizungumza mjini Kigali, amesema hadi sasa, Burundi haijawafikisha kizimbani karibu watu 6,000 wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo. Mutangana amesema Rwanda inafikiria kushirikiana na polisi wa kimataifa (Interpol) kuwakamata watu hao watakapotoka nje ya nchi yao. Mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 yalisababisha vifo vya watu karibu milioni moja, wengi wao wakiwa ni Watutsi.

Mwendesha mashtaka wa Rwanda ameyasema hayo baada ya mkutano wake na Serge Brammertz, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa Inayoshughulikia Masuala Yaliyosalia ya Mahakama za Makosa ya Jinai (IRMCT) yenye makao yake nchini Tanzania.
Brammertz amesema Mutangana amempa ripoti kuhusu jitihada za kuwasaka washukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda.