Rais wa Malawi asema upinzani unataka kumpindua kwa mabavu
(last modified Fri, 07 Jun 2019 08:12:41 GMT )
Jun 07, 2019 08:12 UTC
  • Rais wa Malawi asema upinzani unataka kumpindua kwa mabavu

Rais Peter Mutharika wa Malawi ameutuhumu upinzani nchini humo kuwa unalenga kuipindua serikali yake kwa nguvu.

Rais Mutharika amesema kuwa Lazarus Chakwera kiongozi mkuu wa upinzani na wafuasi wake wanapanga njama ya kuipindua serikali yake.

Upinzani nchini Malawi umekataa kuutambua ushindi wa Mutharika katika uchaguzi wa mwezi Mei. Kwa siku kadhaa wapinzani wamekuwa wakiandamana wakidai kiongozi wao aliibiwa kura.

Chakwera ambaye alishindwa na rais Mutharika kwa kura karibu 190,000 amesema hawezi kukubali na kumtambua mpinzani wake kama rais na ataendelea kushinikiza haki kutendeka.Tayari amewasilisha kesi Mahakamani kupinga ushindi wa Rais Mutharika.

Mutharika aliapishwa siku moja baada ya kutolewa matokeo hayo yaliyokuwa yamecheleweshwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, lakini alitawazwa rasmi kuliongoza taifa hilo kwa muhula mwingine Ijumaa 31 Mei katika Uwanja wa Kitaifa wa Kamuzu katika eneo la Blantyre.

Maandamano ya wapinzani Malawi

Kabla ya hapo, Mahakama Kuu ilitoa agizo la kusitishwa utangazaji wa matokeo ya kura ya rais na kutoa maelekezo ya kuhesabiwa upya kwa kura za theluthi ya maeneo yaliyoshiriki uchaguzi, kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na wapinzani.

Kwingineko, Balozi wa Marekani nchini Malawi Virginia Palmer jana Alhamisi alilazimika kutoka katika makao makuu ya chama cha upinzani cha Malawi Congress Party jijini Lilongwe baada ya polisi kurusha mabomu ya kutoa machozi.

Katika kile kinachoonekana ni hatua ya kuchochea vurugu, balozi huyo alikuwa amekwenda hapo kuzungumza na upinzani. Balozi huyo amedai alikuwa anamuaga kinara wa upinzani kabla ya kurejea nchini Marekani.