Magaidi wa al-Shabaab wateka mji muhimu katika eneo la Puntland, Somalia
Kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab la Somalia limeteka mji mdogo lakini wa kistratajia ulioko kaskazini mashariki mwa eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland.
Wakazi wa mji wa Af Urur wameiambia tovuti ya habari ya Garowe kuwa, magaidi hao wameuteka na kuudhbiti mji huo ulioko yapata kilomita 100 kusini magharibi mwa mji wa Bosaso, baada ya askari wanajeshi wa Puntland kuondoka katika ngome zao kwenye mji huo.
Afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Puntland ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema wanajeshi hao wa Puntland wameondoka kambini hapo ikiwa ni stratajia ya kurejea nyuma ili kupanga mikakati mipya ya kulishambulia na kuliangamiza genge hilo la ukufurishaji.
Julai 20 mwaka jana, genge hilo la ukufurishaji liliteka mji mwingine mdogo lakini wa kistratajia ulioko karibu na eneo la milima ya Galgala, kusini mwa jiji la Bosaso katika eneo hilo lenye mamlaka ya ndani la Puntland, mwezi mmoja baada ya kuuteka mji mmoja wa kistratajia karibu na eneo la Baidoa sambamba na kufunga viwanja zaidi ya 30 vya michezo katika mji mkuu Mogadishu.
Kadhalika mwezi Machi mwaka huu, kundi hilo la kigaidi liliuteka mji mmoja wa kistratajia ulioko kusini magharibi mwa Somalia, baada ya jeshi la Kenya KDF kuwaondoa wanajeshi wake waliokuwa wanaudhibiti mji huo.