Al-Shabaab yawachinja 'majasusi' 5, akiwemo ajenti wa CIA
(last modified Thu, 04 Jul 2019 13:37:50 GMT )
Jul 04, 2019 13:37 UTC
  • Al-Shabaab yawachinja 'majasusi' 5, akiwemo ajenti wa CIA

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limewaua kwa kuwakata vichwa watu watano wanaoshukiwa kuwa majasusi, kusini mwa Somalia.

Tovuti ya habari ya Garowe Online imeripoti kuwa, watuhumiwa hao wa ujasusi waliuawa jana Jumatano katika mji wa Hagar, eneo la Lower Jubba baada ya eti kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa maslahi ya serikali kuu ya Mogadishu, Kenya na Marekani.

Watuhumiwa hao Osman Abdulle (59), Abdikarim Mumin (48), Hassan Barre (35), Omar Hassan (33) na Ahmed Abdullahi (24) walikatwa vichwa kadamnasi ya watu katika Medani ya Hagar eneo la Lower Jubba, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. 

Watuhumiwa wawili kati ya watano waliouawa kikatili hiyo jana wanadaiwa kufanya ujasusi kwa niaba ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA).  

Magaidi wa al-Shabaab wanaendeleza ukatili wao licha ya uepo wa Askari wa Kulinda Amani wa Umoja wa Afrika

Hii sio mara ya kwanza kwa al-Shabaab kutekeleza unyama huo mbele ya familia na watu wa karibu na wahanga wa jinai zao hizo za kutisha.

Hivi karibuni, wazee wanane wa vijiji vya eneo la Galmudug nchini Somalia waliuawa kwa kukatwa vichwa na kundi hilo la kigaidi, eti kwa kuwashawishi wakazi wa maeneo hayo kutolipa kodi na zaka wanazotozwa kwa nguvu na al-Shabaab.

Tags