AU: Vijana wahusishwe ipasavyo katika vita dhidi ya ugaidi
(last modified Fri, 12 Jul 2019 02:27:50 GMT )
Jul 12, 2019 02:27 UTC
  • AU: Vijana wahusishwe ipasavyo katika vita dhidi ya ugaidi

Mjumbe wa Umoja wa Afrika ametoa mwito wa kushirikishwa vijana barabara katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Aya Chebbi, mjumbe wa AU katika masuala ya ugaidi alitoa mwito huo jana Alkhamisi katika mkutano wa kupiga vita ugaidi unaofanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi (Pan African counter-terrorism).

Amesema vita dhidi ya ugaidi vitafanikiwa tu iwapo tabaka la vijana litahusishwa kikamilifu katika kuundwa sera na mikakati ya kufanikisha vita hivyo, kwani vijana wanaunda asilimia kubwa ya watu wa bara hilo.

Chebbi, ambaye pia nimwanaharakati wa masuala ya amani mwenye umri wa miaka 31 raia wa Tunisia ameuambia mkutano huo kuwa, "Serikali zetu zinapaswa kuangalia upya sera zinazowabagua na kuwatenga vijana katika masuala muhimu ya uongozi, na badala yake ziunde sera zinazowapa nafasi za maana vijana katika masuala ya amani na usalama na pia katika vita dhidi ya misimamo ya kuchupa mipaka."

Magaidi wa al-Shabaab wanaotishia usalama na amani Kenya na Somalia

Amesema mikakati ya kupambana na ugaidi imeanza kuzaa matunda katika nchi za Nigeria, Tunisia na Kenya kutokana na serikali za nchi hizo kuwashirikisha vijana katika mikakati yao ya usalama.

Siku ya Jumatano, wakati akihutubia katika ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alionya kuwa ugaidi unatishia uthabiti wa bara la Afrika na kusisitiza kuwa, jinamizi hilo halipaswi kuruhusiwa kudhoofisha mwenendo wa ustawi katika bara hilo.