Mlipuko wa kipindupindu waua makumi Cameroon na Nigeria
Makumi ya watu wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu kaskazini mwa Cameroon tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya nchi hiyo, watu 93 wamefariki dunia huku wengine zaidi ya elfu moja wakiambukizwa ugonjwa huo ndani ya mwaka huu 2019 pekee nchini humo.
Huku hayo yakiripotiwa, watu watatu wapoteza maisha katika jimbo la Adamawa nchini Nigeria kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Hayo yamesemwa na Dakta Bwalki Dalili, Mkurugenzi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii wa Adamawa ambaye ameongeza kuwa, watu 244 wameambukizwa ugonjwa huo.
Dalili amesema wamechukua hatua stahiki kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika maeneo mengine ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Ugonjwa wa kipindupindu husababishwa na baktria waitwao Vibrio cholera na huenezwa kwa kunywa maji yasiyo salama. Dalili za ugonjwa huo ni maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika pamoja na homa.