Katibu Mkuu wa UN atahadharisha kuhusu hatari ya ugaidi barani Afrika
Kupanuka kwa harakati za makundi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya Afrika kumezusha wasiwasi na hofu si baina ya viongozi wa nchi za bara hilo pekee bali hata wa taasisia za kimataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametahadharisha kuhusu athari mbaya za ugaidi barani Afrika. Akizungumzia mgogoro wa ugaidi, Guterres amesema familia ndizo zinazoathiriwa zaidi ya hatari ya ugaidi ambao pia unateteresha usalama na amani. Amesisitiza kuwa, ugaidi haupaswi kudhoofisha mchakato wa ustawi na maendeleo ya bara la Afrika na kwamba kuna udharura wa jamii ya kimataifa kuzihami na kuzisaidia nchi za bara hilo.
Japokuwa nchi za Afrika zinasumbuliwa na changamoto nyingi katika masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiusalama lakini uwepo wa makundi ya kigaidi barani humo na hofu ya kupanuka zaidi harakati za makundi hayo katika nchi mbalimbali limekuwa tatizo kuu linaloshughulisha fikra za viongozi wa Afrika. Kuwepo kwa wanachama wa kundi la Boko Haram katika nchi kadhaa za magharibi mwa afrika hususan Nigeria, harakati za kundi la kigaidi la al Shabab huko mashariki mwa Afrika hasahasa Somalia na mashambulizi ya wapiganaji wa al Qaida huko kaskazini mwa Afrika vinavuruga amani na usalama barani humo. Vilevile kushindwa kundi la kigaidi la Daesh huko Libya na kutokuwepo serikali kuu na utulivu wa kisiasa nchini humo vimewalazimisha wanachama wa kundi hilo kukimbilia katika nchi jirani za Kiafrika na kuhatarisha usalama wa eneo lote la kaskazini mwa bara hilo. Uchunguzi unaonesha kuwa, zaidi ya magaidi elfu kumi wa makundi ya Daesh na al Qaida wamekimbilia maficho barani Afrika.Boko
Makundi hayo yote ya kigaidi yanatumia jiografia, rasilimali na ardhi kubwa ya Afrika kwa ajili ya kutimiza malengo yao sambamba na kufanya jitihada za kuwashawishi vijana wa nchi nyingi maskini za Afrika kujiunga na makundi hayo. Ripoti zinasema vijana wengi wa Kiafrika wamekuwa wakishawishika kujiunga na makundi ya kigaidi kwa kupewa fedha kidogo na ahadi za kupata maisha bora.
Katika miaka ya hivi karibuni nchi za Afrika zimefanya jitihada kubwa za kupambana na makundi ya kigaidi. Hata hivyo kupanuka kwa harakati za makuni hayo, kujitokeza makundi mapya katika maeneo mbalimbali, machafuko ya kisiasa, utendaji dhaifu wa serikali, haja ya kuwepo bajeti kubwa ya masuala ya kijeshi na kutokuwepo ushirikiano wa kikanda katika masuala ya kiusalama na kijeshi vinakwamisha mafanikio ya nchi hizo katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi.
Hali hiyo na hatari ya kupanuka zaidi harakati za makundi ya kigaidi na kuingia katika maeneo mengine ya dunia hususan barani Ulaya, vimewalazimisha baadhi ya viongozi wa nchi za Ulaya kutilia maanani suala la kusaidia mapambano ya nchi za Afrika dhidi ya ugaidi. Katika mkondo huo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitoa pendekezo la kuundwa kikosi cha majeshi ya nchi tano za eneo la Sahel Afrika na wanajeshi wa Ufaransa kwa ajili ya kusimamia operesheni ya kupambana na ugaidi katika eneo hilo. Hata hivyo hatua hiyo haikuzaa matunda yaliyotarajiwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, nchi za Ulaya zinatumia mapambano dhidi ya ugaidi kama kisingizio cha kutuma majeshi zaidi katika nchi za Afrika na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hizo.
Kwa kuzingati ukweli huo nchi za bara Afrika zimechukua uamuzi wa kuzidisha ushirikiano wa kikanda katika masuala ya kijeshi, kiusalama na kiupelelezi na kujaribu kutatua mgogoro wa ugaidi barani humo kupitia ushirikiano wa Kiafrika. Katika uwanja huo Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria anasema: "Kunahitajika jibu la pamoja na lenye uwiano kwa ajili ya kukomsha kabisa vitisho na kuimarisha amani na utulivu wa kikanda."
Kuhusu tishio la ugaidi kwa dunia nzima, Rais Mahamadou Issoufou wa Niger anasema: "Mapambano ya nchi za Afrika dhidi ya ugaidi ni kwa ajili ya dunia nzima, kwa sababu iwapo magaidi wataweza kulidhibiti eneo la Sahel Afrika, hapana shaka kuwa Ulaya pia itapatwa na madhara, na usalama wa dunia kwa ujumla utakuwa hatarini."
Wito uliotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuwasaidia viongozi wa nchi za Afrika katika mapambano yao dhidi ya ugaidi unapata maana zaidi kwa kutilia maanani matamshi ya Rais wa Niger.