Kiongozi mmoja wa Daesh aangamizwa nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54742-kiongozi_mmoja_wa_daesh_aangamizwa_nchini_libya
Kiongozi mmoja wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) ameangamizwa katika shambulizi la anga wapiganaji wanaoijiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 14, 2019 02:19 UTC
  • Kiongozi mmoja wa Daesh aangamizwa nchini Libya

Kiongozi mmoja wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) ameangamizwa katika shambulizi la anga wapiganaji wanaoijiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar.

Duru moja ya habari yenye mfungamano na genge la kigaidi la Daesh imesema kuwa, kiongozi mmoja wa genge hilo ambaye kazi yake ilikuwa ni kusimamia mitandao ya propaganda ya ISIS wameuawa katika shambulio la anga la wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiongozi huyo wa Daesh alikuwa anajulikana kwa jina la kupanga la Abu Aasim al Muhajir licha ya kwamba jina lake la asili alikuwa anaitwa Mohammed bin Ahmed bin Ali al-Fallata.

Abu Aasim ni mzaliwa wa Sudan na alitiwa mbaroni nchini humo kwa tuhuma za kushiriki katika shambulizi la kigaidi. Alifungwa jela na baadaye kuachiliwa huru.

Alipotoka jela alijiunga na genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh na katika miezi ya hivi karibuni alikuwa anaongoza mtandao wa propaganda wa genge hilo la kigaidi nchini Libya.

Mji wa al Fuqaha wa kusini mwa Libya

 

Mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu, kuliripotiwa habari zilizosema kuwa, kwa mara nyingine genge la kigaidi la Daesh (ISIS) lilitumia mwanya uliosababishwa na mapigano kati ya vikosi vya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na vile vya Jenerali Khalifa Haftar kufanya shambulio kusini Libya.

Shirika la habari la Reuters liliripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, watu wanaosadikiwa kuwa wanachama wa Daesh walishambulia mji wa Ghadwa wa kusini mwa nchi na kuua watu watatu, kabla ya kutoroka na kurejea kwenye maficho yao katika mji huo wa jangwani. 

Mwezi wa Aprili pia, kundi hilo lilitangaza kuhusika na mauaji ya watu watatu katika shambulio jingine lililolenga mji wa Fuqaha wa kusini mwa Tripoli.