Machar atoa masharti mapya ya kurejea Sudan Kusini
Kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini, Riek Machar ametoa mwito wa kuondolewa adhabu ya kifungo cha nyumbani, kama moja ya masharti yake ya kurejea mjini Juba.
Katika barua kwa mshauri wa masuala ya usalama wa Rais Salva Kiir, Machar ametoa masharti mengine kadhaa, ambapo anataka akirejea nchini Sudan Kusini aruhusiwe kuzitembelea kwa uhuru nchi wananchama wa Jumuiya ya Kieneo ya IGAD, ambazo ni Kenya, Uganda, Somalia, Eritrea, Djibouti na Ethiopia.
Aidha anataka adhaminiwe usalama wake kabla ya kurejea Juba, mbali na kufutiwa kifungo cha nyumbani. Duru mbalimbali zinadokeza kuwa hivi sasa Machar yuko Khartoum, mji mkuu wa Sudan.
Aprili mwaka huu, Machar alisema hayuko tayari kurejea nchini mwake kwa sasa, huku akitoa mwito wa kuakhirishwa mchakato wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Machar alitazamiwa kurejea nchini Sudan Kusini mwezi Mei mwaka huu, chini ya makubaliano ya amani yaliyosainiwa baina yake na Rais Salva Kiir mwezi Septemba mwaka jana huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, kwenda kuchukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Awali makubaliano hayo yalipaswa kuanza kutekelezwa mwezi Machi mwaka huu kabla ya kuakhirishwa hadi Mei, na hivi sasa utekelezaji wake umeakhirishwa tena hadi mwezi Novemba mwaka huu.