Usitishwaji vita Libya katika Siku Kuu ya Idul Adha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55310-usitishwaji_vita_libya_katika_siku_kuu_ya_idul_adha
Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya (GNA) na ambayo inatambuliwa kimataifa imekubali pendekezo la Umoja wa Mataifa la usitishwaji vita kwa muda wakati wa sherehe za Idul Adha.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Aug 11, 2019 02:28 UTC
  • Usitishwaji vita Libya katika Siku Kuu ya Idul Adha

Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya (GNA) na ambayo inatambuliwa kimataifa imekubali pendekezo la Umoja wa Mataifa la usitishwaji vita kwa muda wakati wa sherehe za Idul Adha.

Serikali ya GNA  imekuwa ikipigana na wanamgambo wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA) ambao wanaongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar kwa miezi kadhaa sasa. Mamia ya watu wameuawa na wengine zaidi ya 100,000 kulazimika kukimbia makazi yao kutokana na vita hivyo.  Haftar, ambaye anapata uungaji mkono wa madola ya Kiarabu kama vile Misri na Saudi Arabia amekataa kujibu pendekezo hilo la usitishwaji vita.

Hayo yanajiri wakati ambao Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao cha dharura kwa ombi la Ufaransa kufuatia kuuawa wafanyakazi watatu wa umoja huo nchini Libya.

Fayez Mustafa al-Sarraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya (GNA)

Wafanyakazi wasiopungua watatu wa Umoja wa Mataifa walioko nchini Libya waliuawa jana jioni katika mripuko wa bomu lililotegwa garini, uliotokea katika mji wa Benghazi kaskazini mwa nchi hiyo.

Stéphane Dujarric msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali shambulio lililolenga wafanyakazi wa UN katika mji wa Benghazi nchini Libya.