Mapigano yaendelea Tripoli licha ya tangazo la usitishaji vita
Mapigano makali yameripotiwa leo huko Tripoli mji mkuu wa LIbya licha ya mapatano ya kusimamisha mapigano katika kusherehekea Sikukuu ya Idhul Adh'ha.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetangaza kuwa, kwa mara ya pili hii leo wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa wamekiuka makubaliano ya kusitisha vita katika Sikukuu ya Idul Adh'ha na wameshambulia uwanja wa ndege wa Mitifa katika mji Tripoli na kusababisha kusitishwa safari za ndege.
Baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii imeripoti kuwa, askari jeshi wa nchi kavu wamewasili katika mji wa Marzouq kusini mwa Libya na kuanza kutekeleza oparesheni dhidi ya kila walichokitaja kuwa ni wapinzani wa Chad na mamluki.
Mapigano hayo yalianza Aprili 4 mwaka huu kwa mashambulizi ya wanamgambo wa kamanda Khalifa Haftar dhidi ya mji wa Tripoli na yangali yanaendelea. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Fayez al Sarraj na wanamgambo wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar jana Jumamosi walikubaliana kusitisha mapigano kwa mnasaba wa kushehekea Sikukuu ya Idul Adh'ha kufuatia pendekezo lililotolewa na Umoja wa Mataifa. Mamia ya watu wameuawa na wengine zaidi ya laki moja wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na vita hivyo.