Rais wa Afrika Kusini kuwasili nchini Tanzania kesho Jumatano
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kesho Jumatano anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili pamoja na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC.
Rais Ramaphosa anatarajiwa kuwa kiongozi wa kwanza wa mataifa ya Afrika ambayo ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC kuwasili nchini Tanzania katika ziara hiyo ambayo itaungana pia na mkutano wa 39 wa SADC unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 na 18 za mwezi huu wa Agosti.
Akiwa nchini Tanzania na kabla ya kuanza mkutano wa SADC, Rais wa Afrika Kusini anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli na kujadili masuala mbalimbali yakiweko ya uhusiano wa pande mbili.
Wakati huo huo, habari kutoka Dar es Salaam, zinasema kuwa maandalizi ya mkutano huo yamekamilika kuhakikisha kuwa, mkutano huo unafanyika kwa mafanikio.
Mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC ambao umepangwa kufanyika kuanzia tarehe 17 mwezi huu wa Agosti jijini Dar es Salaam, utafanyika ikiwa imepita miaka 16 tangu mkutano kama huo ufanyike kwa mara ya mwisho katika katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.