Jenerali Haftar apinga kuongezwa muda wa usitishaji mapigano Tripoli
Kamanda wa kundi la wanamgambo wanaojiita jeshi la kitaifa la Libya amepinga kuongezwa muda wa kusimamisha mapigano nchini humo na kutangaza kuanza tena mashambulizi.
Jenerali Khalifa Haftar amefanya kikao na makamanda anaowaongoza baada ya kumalizika muda wa usitishaji mapigano huko Tripoli na kuwataka kujiandaa kwa ajili ya kuanza mashambulizi mapya dhidi ya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Sirraj. Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya uliwasilisha ombi la kusitishwa mapigano na kufikia mapatano ya kusimamisha vita huko Tripoli siku kadha kabla ya Sikuu ya Idul- Adh'ha; ambapo Jumamosi iliyopita Jenerali Haftar aliafiki ombi hilo.
Wanamgambo hao wanaojiita jeshi la kitaifa la Libya chini ya uongozi wa kamanda Khalifa Haftar tarehe Nne Aprili mwaka huu walianzisha mashambulizi ya kuudhibiti mji mkuu wa Libya, Tripoli. Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyo karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.