UN yalaani mashambulizi dhidi ya vifaa na wafanyakazi wa afya Tripoli
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55413-un_yalaani_mashambulizi_dhidi_ya_vifaa_na_wafanyakazi_wa_afya_tripoli
Umoja wa Mataifa umelaani hujuma dhidi ya vifaa na wafanyakazi wa huduma za afya katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 16, 2019 03:36 UTC
  • UN yalaani mashambulizi dhidi ya vifaa na wafanyakazi wa afya Tripoli

Umoja wa Mataifa umelaani hujuma dhidi ya vifaa na wafanyakazi wa huduma za afya katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Katika taarifa,  mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salame amelaani mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa afya na vifaa vya matibabu yaliyotokea katika mji wa Tripoli.

Mji huo mkuu wa Libya unaendelea kushuhudia mapigano ya kisilaha kati ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na kundi linalojiita Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA), linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar, lenye makao makuu mashariki mwa nchi hiyo.

Tume ya Msaada ya Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL imesema baada ya mapigano kuibuka mjini Tripoli mapema Aprili, mashambulizi zaidi ya 37 yamerekodiwa dhidi ya wafanyakazi na vifaa vya matibabu zikiwemo hospitali na magari ya wagonjwa.

Waziri Mkuu wa  Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya (GNA) Fayez al-Sarraj

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyo karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ikiwa katika mji mkuu Tripoli waziri mkuu wake akiwa ni Fayez al-Sarraj .

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.