Mapigano yaendelea Libya; mji wa Misrata washambuliwa mara 13
Ndege za kivita za kundi la wanamgambo kwa jina la Jeshi la Kitaifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar zimeushambulia mji wa Misrara mara 13.
Ndege hizo zilifanya mashambulizi hayo jana usiku katika mji wa Misrata magharibi mwa Libya na kulishambulia pia jengo la Chuo cha Mafunzo ya Kivita katika mji huo. Itafahamika kuwa, vikosi vya Misrata ni moja ya makundi yanayopigana bega kwa bega na vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya huko magharibi mwa nchi dhidi ya wanamgambo wanaoongozwa na Khalifa Haftar.
Machafuko yalianza kuigubika Libya tangu Aprili nne mwaka huu kufuatia mashambulizi ya wanamgambo wa Jenerali Khalifa Haftar katika viunga vya Tripoli kwa lengo la kuudhibiti mji mkuu huo wa Libya. Wanamgambo hao wanaojiita jeshi la kitaifa la Libya wanapata himaya na uungaji mkono wa Saudi Arabia na Misri. Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ina makao yao Tripoli chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Fayez al Sirraj. Serikali hiyo inaungwa mkono pia na jamii ya kimataifa.