Gadi ya pwani ya Libya yaokoa wahajiri 37
Gadi ya Pwani ya Libya imetangaza kuwaokoa wahajiri haramu wapatao 37 katika pwani ya Khoms. Taarifa ya Jeshi la Majini la Libya imesema wahajiri hao walikuwa ni kutoka nchi 7 za Kiarabu na Kiafrika.
Wahajiri hao wamerejeshwa katika mji wa Khoms ambapo wamepewa huduma za kibinadamu na matibabu kabla ya kukabidhiwa kwa mamlaka ya uhamiaji nchini humo.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri haramu kutoka nchi hasa za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.
Hata hivyo ripoti zinaeleza kuwa, asilimia kubwa ya wahajiri hao huwa hawafiki wanakoelekea, bali huishia mikononi mwa magenge ya magendo ya binadamu, kuzama baharini au kupigwa mnada masokoni na kuuzwa kama watumwa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetangaza kuwa, zaidi ya wahajiri elfu mbili wameaga dunia katika bahari ya Mediterania katika mwaka 2018.
Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa wahajiri 2,262 wamepoteza maisha katika bahari ya Mediterania licha ya mwaka jana wa 2018 kushuhudia kupungua wimbi la wahajiri kuelekea barani Ulaya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka juzi wa 2017 wahajiri 3,139 waliaga dunia katika bahari hiyo tajwa. Mwaka jana wa 2018 watu 113,482 waliwasili katika nchi kadhaa za Ulaya kupitia bahari ya Mediterania na wengine 6,700 walipata hifadhi nchini Uhispania. Hii ni katika hali ambayo mwaka juzi wa 2017 wahajiri 172,301 waliwasili barani Ulaya.