Watu 16 wauawa katika mashambulio dhidi ya vijiji kadhaa nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55506-watu_16_wauawa_katika_mashambulio_dhidi_ya_vijiji_kadhaa_nchini_nigeria
Watu wasiopungua 16 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kushambulia vijiji kadhaa katiika jimbo la Katsina kaskazini mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 21, 2019 07:51 UTC
  • Watu 16 wauawa katika mashambulio dhidi ya vijiji kadhaa nchini Nigeria

Watu wasiopungua 16 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kushambulia vijiji kadhaa katiika jimbo la Katsina kaskazini mwa Nigeria.

Vyombo vya usalama vya Nigeria vimetangaza kuwa, watu waliokuwa na silaha ambao wanasadikiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram wamefanya mashambulio dhidi ya vijiji kadhaa na kufanya mauaji makubwa.

Mashambulio hayo mbali na kupelekea mauaji na majeruhi ya watu yamesababisha pia hasara kubwa kwa mali za watu.

Ingawa hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na mashambulio hayo, lakini mashambulio kama hayo kawaida yamekuwa yakitekelezwa na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Uasi na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram yalianza mwaka 2009 katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria na kisha baadaye kupanua wigo wa mashambulio yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon.

Hadi sasa mashambulio hayo yameshasababisha zaidi ya watu elfu ishirini  na tano kuuawa na wengine karibu milioni tatu kubaki bila makazi, na hivyo kulazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amekuwa akiahidi kila mara kuchukua hatua kali za kupambana na hata kuliangamiza kundi la Boko Haram, lakini hadi sasa ameshindwa kutimiza ahadi yake hiyo, na hivyo kukabiliwa na ukosoaji ndani na nje ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.