Serikali ya Libya yaituhumu UAE kuwa imeshambulia Tripoli kwa mabomu
Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Waziri MKuu Fayez al-Sarraj imesema ndege za kivita za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zimehusika katika kudondosha mabomu katika mji mkuu, Tripoli.
Kwa mujibu wa Idara ya Kamandi ya Oparesheni ya Burkan Alghadab ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya, ndege zisizo na rubani (drone) za Imarati zimedondosha mabomu kusini mwa Tripoli na kupelekea raia watatu kuuawa.
Taarifa hiyo imesema drone hiyo ya kivita ya Imarati imelenga gari walimokuwa wakisafiria raia hao katika eneo la al Karimiya kusini mwa Tripoli.
Imarati ikishirikiana na Misri na Saudi Arabia zinamuunga mkono jenerali muasi Libya, Khalifa Haftar ambaye anaongoza kundi la wanamgambo wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya.
Kuanzi Aprili 4 mwaka huu, wapiganaji wa Haftar wamekuwa wakifanya mashambulizi kwa lengo la kuuteka mji wa Tripoli.
Lakini pamoja na kuwa wanapata uungaji mkono wa madola hayo matatu ya Kiarabu hawajaweza kuuteka mji huo.

Watu zaidi ya 1000 wameuawa katika mji wa Tripoli na wengine wasiopungua 5,500 wamejeruhiwa tangu kuanza mapigano kati ya pande mbili hizo.
Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyoko karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.