Baada ya kudukuliwa mtandao wake, serikali ya Libya yakanusha kuvunjwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55671-baada_ya_kudukuliwa_mtandao_wake_serikali_ya_libya_yakanusha_kuvunjwa
Duru moja ya Baraza la Uongozi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayotambulika kimataifa na ambayo inaongozwa na Fayez al Sarraj imekanusha madai kwamba imevunjwa na mawaziri wake wote kujiuzulu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 29, 2019 07:43 UTC
  • Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayotambuliwa kimataifa
    Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayotambuliwa kimataifa

Duru moja ya Baraza la Uongozi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayotambulika kimataifa na ambayo inaongozwa na Fayez al Sarraj imekanusha madai kwamba imevunjwa na mawaziri wake wote kujiuzulu.

Gazeti la al Rai al Yaum limeinukuu duru moja ambayo haikupenda kutaja jina lake ikizungumzia kuenea taarifa kwenye ukurasa wa Twitter wa Baraza la Uongozi la Serikali ya Umoja wa Kiataifa iliyodai kuwa serikali hiyo imevunjwa na kusema kuwa, mtandao huo umedukuliwa na kundi la jenerali muasi Khalifa Haftar na ndilo lililoandika kwenye ukurasa huo kuwa serikali ya Umoja wa Kitaifa imejiuzulu.

Jenerali muasi Khalifa Haftar katika mazungumzo na mfalme wa Saudi Arabia

 

Katika ukurasa wake wa Facebook, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetoa taarifa maalumu na kusema kuwa, ukurasa wake wa Twitter umedukuliwa na kundi la jenerali muasi Khalifa Haftar na kudai kuwa serikali hiyo imevunjwa wakati si kweli.

Baadhi ya vyombo vya habari hasa televisheni ya al Arabia ya Saudi Arabia, jana vilitoa ripoti pana na kudai kuwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imevunjwa na madaraka yote yamechukuliwa na Jenerali Khalifa Haftar. Itakumbukwa kuwa Saudia, Imarati na Misri ni waungaji mkono wakuu wa jenerali huyo muasi.

Mwezi Aprili mwaka huu, Jenerali Khalifa Haftar alianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, kwa uungaji mkono kamili wa Saudi Arabia, Imarati na Misri, lakini hadi hivi sasa ameshindwa kuudhibiti mji huo.