UN yatahadharisha kuhusu hatari ya kutokea vita vikubwa vya ndani nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55694-un_yatahadharisha_kuhusu_hatari_ya_kutokea_vita_vikubwa_vya_ndani_nchini_libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea kusikitishwa sana na hali inavyoendelea hivi sasa nchini Libya na kutahadharisha kuhusu hatari ya kutokea vita vikubwa vya ndani katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2019 08:52 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu hatari ya kutokea vita vikubwa vya ndani nchini Libya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea kusikitishwa sana na hali inavyoendelea hivi sasa nchini Libya na kutahadharisha kuhusu hatari ya kutokea vita vikubwa vya ndani katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

António Guterres amesema kuwa, kama hatua za kivitendo za kumaliza vita hivyo hazitochukuliwa haraka iwezekanavyo basi Libya itatumbukia kwenye vita vikubwa vya ndani.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amehimiza kutafutwa njia za kisiasa za kutatua mgogoro wa Libya na kukomeshwa mapigano nchini humo na kusema kuwa, hilo halitowezekana bila ya msaada na uungaji mkono kamili wa jamii ya kimataifa.

Vile vile amezitaka pande zote hasimu kusimamisha mapigano huko Libya na ziache kutumia silaha na mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya raia.

António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

 

Aidha ameelezea kusikitishwa kwake na jinsi mamluki walivyomiminwa huko Libya kwa ajili ya kupigana kwa faida ya pande hasimu.

Amma kuhusiana na magendo ya silaha nchini Libya, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande zote kuheshimu azimio nambari 2011 la umoja huo linalopiga marufuku kuingizwa silaha nchini Libya.

Libya haijawahi kushuhdia utulivu wa angalau siku moja tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni za kumng'oa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi. Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zilifanya mashambulizi ya kikatili nchini humo, kuteketeza miundombinu na baadaye kuitelekeza nchi hiyo huku silaha zikiwa zimeenea mikononi mwa makundi mengi hasimu ambayo kila moja linapigania kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo hadi hivi sasa.