Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu dhulma na ukandamizaji Burundi
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema katika ripoti yao waliyoitoa jana kuwa Burundi iko katika hatari ya kukumbwa na wimbi la ukandamizaji mpya wakati ikikaribia kuingia katika uchaguzi mkuu wa 2020. Taarifa hiyo imetolewa huku mgogoro wa kisiasa ulioigubika Burundi ukisalia bila ya ufumbuzi na nchi hiyo ikiwa na Rais anaendelea kujidhihirisha kuwa ni mtawala wa Kimungu.
Serikali ya Burundi ambayo imekataa kushirikiana au kutambua uchunguzi wa Umoja wa Mataifa hata hivyo haijatoa maelezo yoyote kuhusu ripoti hiyo ya wachunguzi wa umoja huo. Ripoti hiyo ya Kamisheni ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi imeeleza kuwa, kuna anga ya woga na ukandamizaji dhidi ya wale ambao hawajaonyesha uungaji mkono wao kwa chama tawala CNDD-FDD. Imeongeza kuwa, polisi, askari usalama na jumuiya ya vijana wa chama tawala kwa jina la "Imbonerakure" wameendelea kukiuka pakubwa haki za binadamu, kufanya mauaji, kupoteza watu, kuwatesa raia na kuwabaka kwa makundi watu wanaodaiwa kumpinga Rais Pierre Nkurunziza.
Doudou Diene Mwenyekiti wa Jopo la Uchunguzi la Umoja wa Mataifa amesema kuwa "hakuna tahadhari ya mapema kuliko hii." Amesema uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 nchini Burundi unashiria hatari kubwa kwa kuzingatia kuwa serikali ya Bujumbura imezidi kuzibana taasisi zisizo za kiserikali na hakuna mfumo halisi wa vyama vingi nchini humo kwa kuwa aghalabu ya vyama hivyo tayari vimesambaratika na kugawanyika.