UN: Wasomali milioni mbili wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa
(last modified Sat, 14 Sep 2019 03:08:03 GMT )
Sep 14, 2019 03:08 UTC
  • UN: Wasomali milioni mbili wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, zaidi ya Wasomali milioni mbili wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa iwapo hawatapata misaada ya haraka wakati huu ambapo nchi za Pembe ya Afrika zinaposumbuliwa na ukame mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa eneo hilo tangu mwaka 2011.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu, Mark Lowcock amesema baada ya safari ya siku mbili nchini Somalia kwamba mavuno ya baina ya kipindi cha mwezi Aprili na Juni mwaka huu nchini Somalia ndiyo mabaya zaidi tangu nchi hiyo ilipopatwa na baa kubwa la njaa hapo mwaka 2011 kutokana na uhaba wa mvua na mafuriko ya msimu wa mvua.

Amesema kutokana na hali hiyo Wasomalia milioni sita hawatakuwa na usalama wa chakula na milioni mbili kati yao watakuwa katika hatari kubwa zaidi iwapo hawatapata misaada ya kibinaamu.

Ukame unatishia maisha ya mamilioni ya Wasomali

Afisa huyo wa UN pia ameonya kuwa matukio yanayohusiana na hali ya hewa "yataendelea kuwa na athari mbaya kwa hali ya kibinadamu nchini Somali."

Mark Lowcock ameongeza kwamba, migogoro ya miongo kadhaa na ukosefu wa uwekezaji vimeharibu sehemu kubwa ya miundombinu ya nchi hiyo ya Afrika na kupunguza uwezo wake wa kukabiliana na migogoro ya aina mbalimbali.

Lowcock ameiomba jamii ya kimataifa kuongeza michango yake kwa wahitaji nchini Somalia ili kuweza kuokoa maisha yao.