Makamanda wa Haftar wauawa karibu na Tripoli, Libya
Wapiganaji watatu wa 'Jeshi la Kitaifa la Libya' wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar wameuawa na wanajeshi wa Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa karibu na mji mkuu Tripoli.
Duru za kijeshi zimeripoti kuwa, wanamgambo hao wakiwemo makamanda wawili wa ngazi za juu waliuawa usiku wa kuamkia leo katika shambulizi la ndege isiyo na rubani katika mji wa Tarhuna, umbali wa kilomita 97.6 kusini mashariki mwa Tripoli.
Ofisi ya Habari ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya imesema shambulizi hilo lililenga gari la wapiganaji wa Haftar katika moja ya ngome zao.
Kuanzia Aprili 4 mwaka huu, wapiganaji wa Haftar kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi wamekuwa wakifanya mashambulizi kwa lengo la kuuteka mji wa Tripoli.
Watu zaidi ya 1000 wameuawa katika mji wa Tripoli na wengine wasiopungua 5,500 wamejeruhiwa tangu kuanza mapigano kati ya pande mbili hizo. Hali kadhalika vita hivyo vimepelekea zaidi ya watu 268,000 kuwa wakimbizi.