Nchi za magharibi mwa Afrika kuchangishana fedha za kupambana na ugaidi
(last modified Sun, 15 Sep 2019 12:17:42 GMT )
Sep 15, 2019 12:17 UTC
  • Nchi za magharibi mwa Afrika kuchangishana fedha za kupambana na ugaidi

Nchi za Magharibi mwa Afrika zimefikia uamuzi wa kuchingashana fedha na kuwa na mfuko maalumu wenye akiba ya dola bilioni moja kwa ajili ya kuendesha mapambano dhidi ya ugaidi.

Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) wamefikia uamuzi huo katika kikao chao cha Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso na kusema kuwa, mfuko huo wa kupambana na ugaidi, utasaidia sana katika vita na magenge ya kigaidi ya magharibi mwa Afrika.

Jean-Claude Kassi Brou, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika amesema kuwa wanachama wa ECOWAS wamefikia uamuzi wa kukusanya haraka fedha hizo ili ziwe msaada katika operesheni za kupambana na magenge ya kigaidi.

Wanachama wa Ecowas

 

Vikundi vyenye mfungamano na magenge ya kigaidi ya al Qaida na Daesh (ISIS) yanafanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi katika eneo la Sahel Africa hususan Mali na Burkina Faso. 

Genge jingine la kigaidi linalofanya jinai kubwa huko magharibi mwa Afrika ni lile la Boko Haram ambalo linafanya jinai hizo katika nchi nne zinazopakana na Ziwa Chad za Nigeria, Cameroon, Niger na Chad.

Nchi 15 ni wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrikak ECOWAS nazo Benin, Burkina Faso, Cabo Verde, Kodivaa (Ivory Coast), Gambia, Ghana, Guinea, Guinea Bissau, Liberia, Mali, Niger, Nigeria, Senegal, Sierra Leone na Togo.