AU yalaani mauaji ya askari wa Burundi nchini Somalia
Umoja wa Afrika umelaani shambulizi la kigaidi dhidi ya askari wa kulinda amani wa Burundi waliokuwa wanahudumu chini ya mwavuli wa Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom).
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat amelaani shambulizi hilo lililotokea Jumamosi iliyopita katika eneo la Hirshabelle, sambamba na kutoa mkono wa pole kwa serikali ya Burundi na kwa familia za wahanga wa shambulizi hilo. Aidha amewatakia ahueni ya haraka majeruhi wa hujuma hiyo.
Taarifa zinasema kuwa, msafara wa askari hao wa Burundi ulishambuliwa wakati ulipokuwa ukirejea kwenye kambi yao kwenye barabara muhimu inayounganisha mji mkuu Mogadishu na Jimbo la Shabelle.
Kundi la wanamgambo wa al-Shabaab lilitangaza kuhusika na shambulio hilo na kueleza kuwa, limefanikiwa kuwaua askari 14 wa Burundi katika shambulio hilo.
Umoja wa Mataifa unafadhili askari hao wa Amisom ambao wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007. Wanajeshi wa Amisom walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone.