Sep 22, 2019 02:31 UTC
  • Makamanda 7 wa kundi la kigaidi la Boko Haram wauawa nchini Nigeria

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, kwa akali limewaua makamanda saba wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika operesheni dhidi ya wanamgambo hao iliyoendeshwa na jeshi la nchi hiyo likishirikiana na majeshi mengine ya nchi kadhaa katika Ukanda wa Ziwa Chad.

Taarifa ya jeshi la Nigeria imeeleza kwamba, operesheni hiyo ya pamoja ya anga ilishambulia ngome za siri za kundi la Boko Haram katika mji mmoja ulioko katika Ukanda wa Ziwa Chad ambapo kwa akali makamanda saba wa wanamgambo hao wameuawa.

Inaelezwa kuwa, waliouawa ni miongoni mwa makamanda muhimu na wa kutegemewa wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Wakati huo huo, Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, limesitisha ushirikiano na Shirika la Kimataifa la  Kupambana na Njaa (Action Against Hunger) linalotoa misaada ya kibinadamu kwa madai kuwa linawapa hifadhi, chakula na dawa magaidi wa Boko Haram, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. 

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Hata hivyo shirika hilo limekanusha vikali madai hayo, baada ya jeshi kufunga ofisi zake mjini Maiduguri bila hata ya kulipatia taarifa.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe harakati zake mwaka 2009, huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na hujuma za genge hilo. Harakati za Boko Haram kwa sasa zimeenea katika nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad. Serikali ya Nigeria inalaumiwa kwa kuzembea katika kukakabiliana na kundi hilo la kigaidi.

Tags