Droni ya Imarati yashambulia Tripoli, watu kadhaa wa familia moja wajeruhiwa vibaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56180-droni_ya_imarati_yashambulia_tripoli_watu_kadhaa_wa_familia_moja_wajeruhiwa_vibaya
Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa droni ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) imeshambulia eneo moja la makazi ya raia katika mji mkuu wa Libya Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 22, 2019 23:13 UTC
  • Droni ya Imarati yashambulia Tripoli, watu kadhaa wa familia moja wajeruhiwa vibaya

Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa droni ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) imeshambulia eneo moja la makazi ya raia katika mji mkuu wa Libya Tripoli.

Shambulio hilo la ndege isiyo na rubani ya Imarati limetekelezwa katika makazi ya raia katika eneo la al Hadaba huko Tripoli katika kumuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar kamanda wa wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya. Watu kadhaa wa familia moja wamejeruhiwa vibaya kufuatia shambulio hilo. 

Katika hali ambayo Imarati inakanusha kuhusika kivyovyote katika mashambulizi huko Libya lakini mwezi Agosti uliopita mmoja wa makamanda wa kundi hilo la Haftar alisema kuwa droni za Imarati zilihusika katika mashambulizi kusini mwa mji mkuu Tripoli. 

Kundi hilo la wanamgambo linaloongozwa na Jenerali Haftar lilianzisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya kusini mwa Libya tangu miezi mitano iliyopita kwa lengo la kuudhibiti mji mkuu Tripoli, hata hivyo limeshindwa kuingia Tripoli licha ya kuungwa mkono kifedha na kijeshi na Imarati na Misri. 

Kamanda Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Imarati na Misri
 

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, hadi sasa karibu watu elfu moja wameuawa, zaidi ya elfu tano kujeruhiwa na wengine zaidi ya laki moja wamelazimika kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi tangu kuanza mashambulizi ya wanamgambo wa Khalifa Haftar  dhidi ya Tripoli Aprili Nne mwaka huu.