Magaidi 30 wa al-Shabaab wauawa na jeshi la Somalia, Lower Shabelle
Makumi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Somalia katika eneo la Lower Shabelle, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Hassan Aden Hashi, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Aprili 12 cha Jeshi la Somalia amewaambia waandishi wa habari leo Alkhamisi kuwa, operesheni hiyo ilifanyika jana Jumatano katika vijiji vya El Salini na Dhanane.
Amebainisha kuwa, "Askari wetu wamewapa kipigo wanamgambo wa al-Shabaab na wamefanikiwa kuua wanachama 30 wa kundi hilo, mbali na kujeruhi wengine 40."
Ameongeza kuwa, jeshi la Somalia limewatia nguvuni wanachama kadhaa wa al-Shabaab sambamba na kunasa magari matatu ya kivita yaliyokuwa yanatumiwa na magaidi hao wakufurishaji.
Operesheni hiyo ya jana imefanyika siku nne baada ya wanajeshi wa Somalia kuua wanachama wengine 13 wa al-Shabaab katika makabiliano ya risasi katika eneo hilo hilo la Lower Shabelle.
Aidha pigo hilo dhidi ya al-Shabaab limejiri siku chache baada ya watu 18 kuuawa nchini Somalia, na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab kushambulia kituo kimoja cha jeshi la Somalia.