Amnesty: Marekani inaua raia katika mashambulizi ya anga Somalia
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema jeshi la Marekani limeua raia wasio na hatia katika moja ya mashambulizi yake ya anga nchini Somalia.
Uchunguzi wa Amnesty International umebaini kuwa, raia watatu wa Somalia waliuawa katika hujuma ya anga ya Machi 18 mwaka huu, huko kusini mwa Somalia. Amnesty imesema watatu hao walikuwa wakulima ambao hawakuwa na mfungamano wowote na magenge ya kigaidi.
Shirika hilo limeikosoa vikali serikali ya Washington kwa kukataa kuchunguza tukio hilo la kuuawa raia katika shambulizi lake la anga. Hata hivyo Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM ilitoa taarifa na kudai kuwa watatu hao walikuwa watu wenye misimamo ya kufurutu ada.
Mwishoni mwa mwaka jana, utafiti uliofanywa na Taasisi ya Hiraal yenye makao makuu yake mjini Mogadishu ulibainisha kuwa, mashambulizi ya anga yanayofanywa kila uchao na Marekani nchini Somalia yameshindwa kulitokomeza au hata kulidhoofisha kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na badala yake yamekuwa na taathira hasi kwa raia wa kawaida.
Taasisi hiyo ilitoa mfano hai wa kutokuwa na tija mashambulizi ya anga ya Marekani, kwa kuashiria kuuawa raia wasiopungua 60 wakati Marekani ilipofanya hujuma ya anga mwezi Oktoba mwaka uliopita katika mkoa wa Mudug katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Kikosi cha Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM kilitoa taarifa kikidai kuwa shambulizi hilo lililenga maficho ya al-Shabaab. Nayo taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilitoa taarifa kinzani iliyosema kuwa shambulio hilo lilifanyika katika eneo la Harardhere ambako Marekani inatoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa Somalia, na kwamba makurutu 60 waliuawa kwa 'bahati mbaya'.