Wapiganaji wawili wa Jenerali Haftar wauawa karibu na mji mkuu wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56374-wapiganaji_wawili_wa_jenerali_haftar_wauawa_karibu_na_mji_mkuu_wa_libya
Wapiganaji wawili wa jenerali muasi Khalifa Haftar wameuawa katika mapigano na wanajeshi wa serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa kimataifa, karibu na mji mkuu wa Libya, Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 02, 2019 07:21 UTC
  • Wapiganaji wawili wa Jenerali Haftar wauawa karibu na mji mkuu wa Libya

Wapiganaji wawili wa jenerali muasi Khalifa Haftar wameuawa katika mapigano na wanajeshi wa serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa kimataifa, karibu na mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Kwa upande wao, wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati, Misri na Ufaransa wamedai kuwa wameangamiza kifaru kimoja na kuteka gari moja la kijeshi pamoja na kuua wanajeshi kadhaa wa serikali ya Umoja wa Kitaifa katika mapigano yaliyotokea alfajiri ya jana. Hata hivyo hadi wakati wa kuandaa taarifa hii, serikali ya Tripoli ilikuwa haijathibitisha wala kukanusha madai hayo.

Wapiganaji wa Khalifa Haftar wamekiri kwamba wamepoteza wapiganaji wao wawili kwenye mapigano hayo yaliyotokea kusini mwa Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Mapigano mjini Tripoli, Libya

 

Kwa karibu miezi sita sasa, jenerali muasi Khalifa Haftar anaendesha vita dhidi ya serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa. Mwezi Aprili mwaka huu, Jenerali Haftar alitoa amri kwa wanamgambo wake kuushambulia kwa pande zote mji mkuu wa Libya, Tripoli kama juhudi za kutaka kuuteka mji huo na kuiangusha serikali ya Umoja wa Kitaifa. Licha ya kupata uungaji mkono wa kila upande kutoka kwa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na Ufaransa, lakini jenerali huyo muasi ameshindwa kuuteka mji huo. Hatua hiyo ya Haftar ya kuanzisha vita dhidi ya  Tripoli imeshapelekea maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa na wengine wapatao laki moja na 20 elfu kuwa wakimbizi.

Libya haijawahi kushuhudia utulivu wa angalau siku moja tangu ulipoangushwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.