Oct 06, 2019 12:00 UTC
  • Magaidi wa Boko Haram waua watu 27 Nigeria

Watu 27 wamepoteza maisha kaskazini mashariki mwa Nigeria kufuatia shambulizi la kigaidi ambalo limetekelezwa na kundi la Boko Haram linalofungamna na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh).

Kwa mujibu wa taarifa, siku ya Jumamosi magaidi wa Boko Haram walitekeleza shambulizi la kuvizia dhidi ya msafara wa kijeshi karibu na kijiji cha Mauro, eneo la Bani Sheikh katika jimbo la Borno ambapo raia 17 na askari 11 wameuawa.

Afisa mmoja wa kijeshi ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa, katika hujuma hiyo magaidi walipora bunduki 11 aina ya AK 47, makombora na lori moja lililokuwa limejaa shehena ya silaha.

Aidha imearifiwa kuwa wanajeshi wawili wa Nigeria walitoweka baada ya shambulizi hilo.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.

Serikali ya Nigeria inalaumiwa kwa kuzembea katika kukakabiliana na kundi hilo la kigaidi jambo ambalo limepelekea liendelee kutekeleza mashambulizi katika nchi zilizotajwa.

Tags