Oct 13, 2019 07:58 UTC
  • Shambulizi dhidi ya msikiti laua watu 15 Burkina Faso

Kwa akali watu 15 wameuawa baada ya watu waliobeba silaha kushambulia msikiti mmoja kaskazini mwa Burkina Faso.

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, shambulizi hilo lilitokea wakati wa Sala ya Ijumaa katika kijiji cha Salmossi eneo la Oudalan, mpakani mwa nchi hiyo na Mali.

Genge la watu wasiojlikana liliwamiminia risasi waumini wa Kiislamui waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya Sala ya Ijumaa na kuua 15 na kujeruhiwa wengine kadhaa.

Maafisa wa serikali ya Burkina Faso wanasema, kuna uwezekano wa kuongezeka idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi hayo.

Magenge ya magaidi na waasi yanayoendelea kuhatarisha usalama wa Burkina Faso

Mwezi uliopita wa Septemba, watu 30 waliuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya kigaidi yaliyotekelezwa nchini humo.

Tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa, magenge ya kigaidi yameongeza mashambulizi yao katika maeneo mbalimbali hasa ya kaskazini na mashariki mwa Burkina Faso. Hadi hivi sasa watu wasiopungua 570 wameshauawa kwenye mashambulio hayo.

Tags