Al-Shabaab yateka mji wa kistratajia karibu na Mogadishu
Kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab la Somalia limeteka mji wa kistratajia ulioko karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
Mashuhuda wanasema magaidi hao wameuteka na kuudhibiti mji wa el-Gelow ulioko katika eneo la Shabelle ya Kati, yapata kilomita 30 kutoka mji mkuu Mogadishu.
Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi hao wameuteka mji huo baada ya Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) kuondoa askari wake katika eneo hilo.
Msemaji wa genge hilo la ukufurishaji, Abdiaziz Abu Musab amedai kupitia radio yao ya kipropaganda ya Andalus kuwa, wanachama wa kundi hilo wamefanikiwa kuuteka mji huo muhimu bila ugumu wowote, baada ya wanajeshi wa serikali kutoroka walipoona wanamgambo hao wanaukaribia.
Kutekwa kwa mji huo ni muendelezo wa kutekwa kwa makumi ya miji muhimu ya Somalia na wapiganaji wa al-Shabaab licha ya uwepo vikosi vya kulinda amani vya kimataifa.
Juni mwaka huu, genge hilo la ukufurishaji liliteka mji mwingine mdogo lakini wa kistratajia ulioko karibu na eneo la milima ya Galgala, kusini mwa jiji la Bosaso katika eneo hilo lenye mamlaka ya ndani la Puntland, mwezi mmoja baada ya kuuteka mji mwingine wa kistratajia karibu na eneo la Baidoa sambamba na kufunga viwanja zaidi ya 30 vya michezo katika mji mkuu Mogadishu.
Kadhalika mwezi Machi mwaka huu, kundi hilo la kigaidi liliuteka mji mmoja wa kistratajia ulioko kusini magharibi mwa Somalia, baada ya jeshi la Kenya KDF kuwaondoa askari wake waliokuwa wanaudhibiti mji huo.